Thursday, August 25, 2011

VIWANGO VIPYA VYA UBORA WA SOKA DUNIANI, UHOLANZI YAIONDOA HISPANIA KILELENI, BRAZIL YAANGUKA NAFASI MBILI, TANZANIA YAPANDA MBILI

Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Uholanzi
Uholanzi imeipiku Hispania katika nafasi ya kwanza ya ubora Fifa wa kusakata soka duniani, huku Englan ikipanda nafasi mbili juu hadi ya nne.
Hispania mabingwa wa soka duniani na Ulaya, wameporomoka hadi nafasi ya pili baada ya kupoteza pointi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Italia.
England, licha ya mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Uholanzi kuahirishwa, imepanda kwa sababu Brazil ilifungwa na Ujerumani.
Jamhuri ya Ireland imepaa nafasi mbili hadi ya 31, Scotland imeruka nafasi sita na sasa inashikilia nafasi ya 55, Ireland Kaskazini nayo imefanikiwa kwenda nafasi tatu zaidi hadi ya 59, lakini Wales imeporomoka hadi nafasi ya 117.
Kwa kushika nafasi hiyo ya kwanza kwa mara ya kwanza, Uholanzi inakuwa ni taifa la saba kushikilia nafasi hiyo ya juu kisoka duniani zikiwemo - Argentina, Brazil, Ufaransa, Ujerumani na Italia ambazo ziliwahi kukalia kiti hicho.
Hispania ilikuwa inashikilia nafasi ya juu tangu mwezi wa Julai mwaka 2010 kufuatia ushindi walioupata wa Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi nchini Afrika Kusini.
Ujerumani inashikilia nafasi ya tatu, wakati Uruguay ndiyo nchi ya Amerika Kusini iliyo nafasi ya juu kwa dunia ikishika nafasi ya tano kutokana na kushinda Kombe la Copa America hivi karibuni nchini Argentina, wakati Brazil ipo nafasi ya sita.
Italia, Ureno, Argentina na Croatia wamefanikiwa kushikilia nafasi 10 za juu.
Wakati huo huo Tanzania imepanda nafasi mbili katika viwango hivyo vipya kutoka nafasi ya 127 mpaka nafasi ya 125. Viwango vya ubora wa soka vya Fifa vinatokana na kukusanya matokeo, umuhimu wa mechi zilizochezwa na ubora wa timu pinzani.

No comments:

Post a Comment