Wednesday, September 28, 2011

AFRIKA KUSINI KUANDAA AFRICA CUP OF NATIONS 2013

MOJA YA VIWANJA VITAKAVYOTUMIKA KWENYE AFCON 2013
UWANJA WA CAPE TOWN 
Libya imeichia nafasi ya kuandaa mashindano hayo kutokana na hali kutokuwa shwari nchini humo.
Badala yake Libya itaandaa mashindano ya mwaka 2017, ambayo ilikuwa awali yafanyike nchini Afrika Kusini.
Kubadilishana huko ni makubaliano baina ya nchi hizo mbili ambayo yalifahamika wiki mbili zilizopita.
Wakati huo Caf ilisema tangazo hilo limetolewa mapema mno, huku Nigeria na Algeria pia zilionesha nia ya kuandaa.
Nigeria ilitajwa kuwa nchi itakayosubiri wakati Caf ilipotoa tangazo la awali kuhusu wapi mashindano ya kuuanzia mwaka 2010 - 2014 yatakapofanyika.
Lakini uamuzi wa kufanya mashindano hayo Afrika Kusini, uliidhinishwa na mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Caf unaofanyika mjini Cairo.
Afrika Kusini pia itachukua nafasi ya Libya kuandaa michezo ya mwaka 2014 ya Mataifa ya Afrika, kwa wachezaji wanaotimua ligi za nyumbani.
Mapema mwaka huu waliandaa pia mashindano ya vijana ya Afrika chini ya miaka 20, ambayo Libya ilishindwa kuandaa.
Caf pia ilitangaza nchi mbalimbali zitakazoandaa mashindano kadha makubwa.
Namibia itandaa mashindano ya Wanawake ya mwaka 2014 ya Ubingwa wa Afrika na Niger itachukua jukumu la kuandaa mashindano ya mwaka 2015 chini ya umri wa miaka 17 .
Senegal itakuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2015 chini ya umri wa miaka 20, wakati Madagascar itakaribisha nchi nyingine katika kuwania ubingwa wa mashindano ya umri wa chini ya miaka 17 ya mwaka2017.

Thursday, September 15, 2011

YANGA KATIKA MTIHANI MWENGINE KWA LYON LEO!



Yanga hii leo wanateremka kwenye nyasi bandia za Azam kumkabili African lyon katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara.
Yanga watakuwa wanasaka ushindi wao wa kwanza toka wamfunge simba katika fainali ya Kagame Cup, huku wakihangaika kujinasua toka mkiani. Leo watashuka bila ya mshambuliaji wake waliyo mfungia kwa utovu wa nidhamu Jerry Tegete.
Afican lyon watateremka katika dimba la Azam wakiwa na dhamira ya kuendelea kuitibulia yanga huku nao wakitaka kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi kwa kuibuka na ushindi hii leo.
Katika mchezo uliochezwa jana Simba waliichapa goli moja timu ya Polisi Dodoma, goli lililo fungwa na Kago.


MSIMAMO WA VPL.Kwenye Mabano Idadi ya Mechi Zilizochezwa.
1. Simba SC (5) 13
2. JKT Ruvu (5) 9
3. Mtibwa Sugar ( 5) 8
4. Moro United (5) 8
5. Azam FC (5) 8
6. Toto Africa (5) 7
7. JKT Oljoro ( 5) 6
8. Africa lyon (4) 5
9. Coastal Union (5) 4
10. Villa Squad (5) 4
11. Kagera Sugar (5) 4
12. Ruvu Shooting (5) 4
13. Polisi Dodoma (5) 3
14. Yanga SC (4) 3

CHANGIA KUSAIDIA WAATHIRIKA WA AJALI YA MELI YA MV. SPICE ISLANDERS

Wednesday, September 14, 2011

BOAS: CHELSEA 'ITAITUNGUA' MAN UTD

Andre Villas Boas
Meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas amekiri kikosi chake kitakabiliana na " changamoto tofauti" watakapojimwaga uwanja wa Old Trafford siku ya Jumapili kuikabili Manchester United.
David Luiz na Juan Mata walifunga mabao wakati Chelsea ilipoilaza Bayer Leverkusen mabao 2-0 wakati wa mechi yao ya ufunguzi kuwania Ubingwa wa Ulaya siku ya Jumanne.
Akiwa jicho moja ametumbulia mechi ya Jumapili, Villas-Boas alimpumzisha nahodha John Terry na Frank Lampard alikuwa katika benchi la wachezaji wa akiba.
Villas-Boas amesema: "Tutakwenda kujaribu kushinda. Itakuwa mechi nzuri sana nyakati hizi ligi ikiwa katika hatua za mwanzo."
Ameongeza: "Tunakabiliana na United pengine katika kipindi kizuri zaidi kilichojaa motisha, vipaji na mbinu nyingi za kupendeza za uchezaji.
Chelsea walionekana kun'gara muda mwingi wa mchezo dhidi ya timu hiyo ya Ujerumani, huku mshambuliaji anayechezea pia timu ya Taifa ya England chini ya umri wa miaka 21 Daniel Sturridge akiwa anaisumbua sana ngome ya Bayer Leverkusen kabla Luiz kufunga bao katika dakika ya 67 na Mata akaihakikishia ushindi kwa kupachika bao la pili zikiwa zimesalia dakika chache kabla mpira haujamalizika.
Matokeo hayo yamemfurahisha sana Villas-Boas, ambaye alisema: "Tulipata nafasi nyingi katika mchezo huo na tulistahili kushinda.

PAT RICE AWAPA MATUMAINI WAPENZI WA ARSNAL

Robin van Persie
Meneja msaidizi wa Arsenal Pat Rice, anaamini sare dhidi ya Borussia Dortmund katika mechi ya kwanza ya patashika za Ligi ya Ubingwa wa Ulaya ni muelekeo mzuri wa timu hiyo kuanza kubadilika msimu huu.
Arsenal walionekana wameshinda mechi hiyo na kuzoa pointi tatu katika Kundi F hadi dakika ya 88 ambapo Ivan Perisic aliisawazishia Dortmund.
Lakini Rice, alipoulizwa iwapo Arsenal sasa imeanza kubadilika alisema: "Sana tu.
"Inaonekana ni hivyo, hasa ushindi dhidi ya Swansea siku ya Jumamosi, ndio tulianza msimu. Wachezaji tulionao ni wazuri, wazuri sana, ni wachezaji wazuri sana." Aliongeza Rice.
Arsenal walikuwa na hali ngumu hasa robo ya msimu huu kufuatia kuyumbayumba katika mechi za ligi baada ya kutoka sare na Newcastle na baadae wakapoteza mechi dhidi ya Liverpool na Manchester United - ambapo katika uwanja wa Old Trafford walibugizwa mabao 8-2.
Hata kufuzu kwa Arsenal katika Ubingwa wa Ulaya walipoishinda Udinese kwa jumla ya mabao 3-1, bado timu ilikuwa ikiyumba.
Hata hivyo mwishoni mwa dirisha la usajili, wakati Cesc Fabregas na Samir Nasri walipouzwa na wakawasajili Per Mertesacker, Mikel Arteta na Yossi Benayoun, mechi ya Jumamosi ya Ligi Kuu ya England walipoishinda Swansea, Rice anaamini Arsenal sasa ipo katika mchakato wa kujengeka.
Na kocha huyo amekuwa na kauli ya matumaini kufuatia sare dhidi ya Dortmund.
Robin van Persie alionekana kuifagilia njia ya ushindi Arsenal katika mechi ya ufunguzi ya kundi la F kwa kumalizia vizuri pasi aliyotanguliziwa na Theo Walcott lakini bao maridadi la Perisic likawanyima Arsenal pointi tatu.
Naye kocha wa Dortmund Jurgen Klopp amesema timu yake ilistahili kupata sare baada ya jitahada kubwa walizofanya.
"Ilikuwa ni mechi nzuri, lakini wakati mwengine kandanda ndivyo ilivyo," alisema Klopp. "Tulicheza vizuri, vizuri sana kwa muda wote wa dakika 90.

KAGO AIPAISHA TENA SIMBA

Uhuru Suleimani wa Simba (kushoto) akiruka daluga la beki wa Polisi Tanzania, Nassor Mhagama.
Shujaa wa Msimbazi, Gervas Kago.
Katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliochezwa kwenye uwanja wa Azam,uliopo Chamazi jijini Dar-es-Salaam. Simba imeshinda 1-0.

REAL MADRID KUINGIA NA 'UZI' MWEKUNDU LIGI YA MABINGWA ULAYA

MASHABIKI WA LIVERPOOL WATAFURAHI KUMONA KIPENZI CHAO XABI ALONSO NDANI YA JEZI NYEKUNDU TENA

VILABU KUPATA MGAO LIGI YA MABINGWA ULAYA

Timu zitakazoshiriki kwenye michuano ya ligi ya mabingwa kwenye hatua ya makundi zina uhakika wa mgao wa Euro Milioni 7.2 kwa kila timu mgao ambao unatokana na mapato yanayopatikana toka kwenye vyanzo mbalimbali vya udhamini.
Mgawanyo huu unaonyesha kuwa timu itakayotwaa ubingwa itajipatia Euro Milioni 31.5, Hii ni kwa mujibu wa mfumo wa ugawanywaji wa mapato ya ligi ya mabingwa kwa msimu wa 2011/12.
Kila klabu kati ya vilabu 32 vinavyoshiriki itapata bonus ya ushiriki ambayo ni Euro milioni 3.9, na zaidi ya hapo kila timu itapata mgao wa kila mechi ambao ni Euro 550,000 kwa kila mechi ambayo timu inacheza , sambamba na hizo kuna mgao mwingine wa Euro 800,000 kwa kila mchezo ambao timu inashinda , Euro 400,000 kwa kila mechi ambayo timu inatoa sare kwenye hatua ya makundi.
Timu zitakazofuzu kuingia hatua ya 16 bora zitapata Euro Milioni 3 kila moja na zinazoingia robo fainali zitapata Euro milioni 3.3 na hatua ya nusu fainali itazipatia timu zitakazoingia Euro milioni 4.2 huku washindi wa fainali wakipata Euro Milioni 9 na washindi wa pili watapata Euro milioni 5.6 .
Katika makadirio hayo , jumla ya Euro milioni 55 zitaelekezwa kwenye mechi za mtoano ambapo kila timu inayoshiriki itajipatia Euro milioni 2.1 . Pamoja na hayo , kama ilivyokuwa kwenye michuano ya misimu ya 2006-09 , Euro milioni 10 zitawekwa kando kwa ajili ya timu zitakazotolewa kwenye hatua ya mtoano wa kufuzu na timu zitakazotolewa na kucheza ligi ya Europa .
Jumla ya asilimia 75% ya mapato yote yanayotokana na haki za matangazo na mikataba ya kibiashara inayofikia kitita cha Euro Milioni 530 itaenda kwa vilabu huku kiasi kinachobaki ambacho ni asilimia 25% zitabaki kwa ajili ya soka la ulaya ambako UEFA itazitumia kugharamia uendeshwaji wa michuano hii ya ligi ya mabingwa huku fedha nyingine zikilipwa kwa vyama wanachama wa UEFA, vilabu na ligi mbalimbali.
Jumla ya asilimia 82% ya mapato yote yanayopatikana toka kwenye mkondo huo huo wa milioni 530 zitaenda kwa vilabu , huku 18 ikitumika kwenye uendeshwaji wa UEFA kwa ujumla .
Kiasi cha Euro milioni 341 ambazo zimebakia toka kwenye mkondo wa soko la televisheni zitagawanywa kwa kuendana na thamani ya kila soko la televisheni kama inavyowakilishwa na vilabu vinavyoshiriki kwenye ligi ya mabingwa kwenye hatua ya makundi la ulaya ambako UEFA itazitumia kugharamia uendeshwaji wa michuano hii ya ligi ya mabingwa huku fedha nyingine zikilipwa kwa vyama wanachama wa UEFA , vilabu na ligi mbalimbali.
Jumla ya asilimia 82% ya mapato yote yanayopatikana toka kwenye mkondo huo huo wa milioni 530 zitaenda kwa vilabu , huku 18 ikitumika kwenye uendeshwaji wa UEFA kwa ujumla .
Kiasi cha Euro milioni 341 ambazo zimebakia toka kwenye mkondo wa soko la televisheni zitagawanywa kwa kuendana na thamani ya kila soko la televisheni kama inavyowakilishwa na vilabu vinavyoshiriki kwenye ligi ya mabingwa kwenye hatua ya makundi kwenda mbele na pia zitagawanywa kwa timu kadri zinavyoshiriki toka kwa vyama husika vya nchi vya soka.

VAN DER VAART ACHUKIA KUACHWA EUROPA

Rafael van der Vaart
Kiungo mshambuliaji wa Tottenham Rafael van der Vaart amesema amekasirika kuachwa katika kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki Ligi ya Europa.
Van der Vaart alitoka akichechea wakati Spurs iliposhindiliwa mabao 5-1 na Manchester City na awali ilielezwa asingeweza kucheza kwa muda wa wiki sita akiuguza msuli wa paja.
Lakini licha ya sasa akiwa anatarajiwa kupona na kuweza kucheza mechi dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili, kuenguliwa kwake kuna maana mchezaji huyo atakosa mechi sita za makundi za ligi ya Europa.
"Spurs wangeweza kushauriana nami," alieleza katika mtandao wake rasmi binafsi.
Amesema zaidi: "Nadhani ni suala la aina yake."
Hata hivyo amesema hayo anayapa kisogo na anajiandaa kwa pambano dhidi ya Liverpool na ameonesha matumaini atakuwa amepona kabisa hadi wakati huo.
Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid alikosa kuiwakilisha nchi yake ya Uholanzi kwa mashindano ya kufuzu kwa Euro 2012 na pia hakupangwa katika mechi ya kwanza kwa Spurs kushinda msimu huu dhidi ya Wolves siku ya Jumamosi.
Meneja wa Spurs Harry Redknapp anakusudia kuchezesha damu changa kama Harry Kane, Tom Carroll na Jake Livermore katika Ligi ya Europa ili kukiweka kikosi chake tayari kwa ajili ya patashika za Ligi Kuu ya England.
Spurs wataanza mtanange wa Ligi ya Europa League dhidi ya PAOK Salonika nchini Ugiriki siku ya Alhamisi.
Iwapo watafanikiwa kusonga mbele katika hatua ya makundi, wataruhusiwa kusajili wachezaji wengine watatu wapya.

SIMBA, YANGA HEBU WAIGENI HAWA.....

Napenda niwaulize wadau kama kweli ni haki kwa Timu za Simba na Yanga kuufanya uwanja wa Azam FC kuwa kama uwanja wao wa nyumbani!! La hasha, kwa mimi nitasema si haki, ni kitendo cha aibu sana kwa timu hizi mbili kubwa ambazo kama tunavyojuaona ni jinsi gani zilivyo vilabu kongwe hapa nchini lakini havina viwanja vyao vya kuweza kucheza mechi zao za ligi za nyumbani na za kimataifa.
Tunawaomba Viongozi wa timu hizi mbili mlio madarakani kw sasa muone hili ni kama changamoto kwenu kwa timu changa imeweza kuwa na uwanja wake, na timu zenu zikajikuta mnaenda kucheza kwenye uwanja huo, ni fedheha sana kwenu.
"USHAURI WA BURE VIONGOZI JITAHIDINI KUJALI MASLAHI YA TIMU ZENU"

TIMU YA KIKAPU YAENDA NAIROBI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Mussa Mziya (kulia) akikabidhi bendera ya Taifa kwa nahodha wa timu ya wachezaji wa mpira wa kikapu chini ya miaka 16 Mrumbia Issa jijini Dar es Salaam Jana Jumanne Septemba 13, 2011. Timu hiyo imeondoka leo Jamatano Septemba 14, 2011 kwenda Nairobi, Kenya, kushiriki fainali za timu kutoka ukanda wa Coca-Cola wa Afrika Mashariki, Kati na Afrika Magharibi (CEWA). Nyota wa fainali hizo watachaguliwa kwenda Marekani kwenye mafunzo zaidi chini ya udhamini wa Coca-Cola kupitia kinywaji chake cha Sprite.

Tuesday, September 13, 2011

OKWI KUIWAHI MECHI YA KESHO

Mshambuliaji Emmanuel Okwi hivi sasa yupo kwenye uwanja wa ndege wa O Tambo jijini Johanesburg nchini Afrika ya Kusini akisubiria ndege ya kuja nchini Tanzania. Okwi alikuwa kwenye michuano ya ALL African Games akiwa na nchi ya Uganda, taarifa zilizoifikia Blog hii zinasema uongozi wa Simba umelazimika kumtumia Tiketi ya ndege ili auwahi mchezo wa kesho wa ligi kuu dhidi ya Polisi Dododma.

RIO FERDINAND AJIBU MASWALI YA MASHABIKI WAKE KWA NJIA YA TWITTER!

TWITTER Q&A NA RIO FERDINAND
Qn: Kama unapewa nafasi ya kuchagua kiungo bora kati ya Scholes, Gerrard, au Xavi utamchagua nani?
Rio: Paul Scholes a.k.a Satnav
Qn: Ni mafanikio makubwa unayojivunia katika maisha yako nje ya soka?
Rio: Namba 1 ni kupata uwezo wa kuwanunulia nyumba nzuri wazazi wangu.
Qn: Ni wachezaji gani ambao best professional na umewahi kucheza nao?
Rio: Gary Neville, Mikael Silvester na Ryan Giggs.
Qn: Uliumia zaidi kumuona mchezaji gani akihama Manchester United?
Rio: Cristiano Ronaldo, mchezaji bora, rafiki mzuri na alikuwa ananifurahisha sana, I miss him.
Qn: Mchezaji gani ambaye umewahi kupata tabu sana kumkaba katika soka?
Rio: Louis Saha ni kiboko alikuwa akinipa taabu sana zaidi tulipokuwa kwenye mazoezi ya Manchester United.
Qn: Top 3 ya viwanja ambavyo ni vigumu kucheza?
Rio: Uwanja wa Stoke, Middlesborough na Wolves, tena zaidi pitch zinapokuwa ngumu.
Qn: Mechi ngumu zaidi ya ugenini katika hatua ya makundi ya Champions league?
Rio: Mechi dhidi ya Villareal na ile dhidi ya Lille zilikuwa ngumu sana.
Qn: Kama ukipata nafasi ya kurudisha nyuma moja ya nyakati zilizopita katika maisha yako ndani ya soka, ungependa wakati upi ujirudie?
Rio: Mchezo wa fainali ya Champions league dhidi ya Chelsea in 2008, au mechi ya kwanza kuvaa na kucheza katika timu ya taifa na West Ham, au kufunga kwenye World Cup.
Qn: Je ungeendelea kucheza soka kama mishahara ya wachezaji wote itapunguzwa kuwa ya wastani mdogo?
Rio: Nitacheza kwa hali yoyote, haijalishi nalipwa kiasi gani.Naupenda huu mchezo.
Qn: Kiatu kipi unachokipenda zaidi na umewahi kukichezea?
Rio: Nike tiempo, kilaini na kipo comfortable kukichezea.
Qn: Nafasi gani unayopenda kucheza tofauti na ulinzi uwanjani?
Rio: No.10, kama Zidane au Bergkamp.

WASHIRIKI WA SHINDANO LA THE GUINNESS FOOTBALL CHALLENGE WAENDA 'BONDENI'

 Vijana 16 waliopata nafasi ya kushiriki katika shindano la kuonyesha kipaji na uelewa wa mambo ya soka wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuondoka kuelekea njini Johannesburg, Afrika Kusini kwa ajili ya kurekodi tangazo la promosheni la kipindi chaTelevisheni cha Guinness Football Challenge, watakuwa wakishindania dola 50,000 kila wiki.
 Hapa wakielekea kupanda ndege ya shirika la ndege la South Africa Airways kwa ajili ya kurekodi tangazo la televisheni kwa ajili ya kipindi cha Guinness Football Challenge.
Vijana wakielekea uwanja wa ndege tayari kwenda south africa na Ndege ya South African Airline

TIKETI ZA MECHI ZA SIMBA NA YANGA HAZITOUZWA CHAMANZI....

Tiketi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zinazohusisha timu za Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam hazitauzwa uwanjani. Lengo ni kuwaondolea usumbufu mashabiki ambao wanakwenda kwenye mechi hizo na kukuta tiketi zimekwisha, hivyo kuweza kuwa chanzo cha vurugu.
Ili kujiridhisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilifanya uhakiki na kubaini Uwanja wa Azam una uwezo wa kuchukua watazamaji 5,000 tu na si 7,000 kama ilivyoelezwa awali. Hata hivyo lengo la mmiliki wa uwanja huo ni kuongeza viti hadi kufikia 7,500.
Kwa mantiki hiyo tiketi zitakazouzwa kwa mechi za Yanga na Simba kwenye uwanja huo ni 5,000 tu. Vituo vya kuuzia tiketi hizo siku moja kabla ya mchezo na siku yenyewe ya mchezo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha Mafuta cha OilCom kilichoko Ubungo na Mbagala Rangitatu.
Viingilio kwa mechi za timu hizo zitakazochezwa Uwanja wa Azam ni sh. 20,000 kwa jukwaa kuu lenye uwezo wa kuchukua watazamaji 400 wakati majukwaa ya kawaida itakuwa sh. 7,000. Ili kuhakikisha idadi ya mashabiki haizidi uwezo wa uwanja hakutakuwa na tiketi za bure (complimentary).
Hivyo kutokana na kuwepo vituo vya kuuzia tiketi katika maeneo yaliyotajwa, mashabiki ambao watakosa tiketi hawana sababu ya kwenda uwanjani. Simba na Yanga zitaanza kuutumia uwanja huo kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa Simba kuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma wakati siku inayofuata Yanga itakuwa mgeni wa African Lyon.

LOUIS SENDEU ASHITAKIWA TENA!

Louis Sendeu - Afisa Habari wa Klabu ya Yanga.

Sekretarieti ya TFF itawasilisha mashtaka dhidi ya Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi inayoongozwa na Kamishna wa Polisi mstaafu Alfred Tibaigana kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi.
Mara baada ya mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Sendeu aliita mkutano na waandishi wa habari na kumshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao.
Aliongeza kuwa anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba, kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima si halali na alifanya hivyo kwa lengo la kuisadia Simba ili iendelee kukaa kileleni mwa ligi.
Kauli ya Sendeu ililenga kumjengea chuki Mahagi mbele ya mashabiki wa Yanga kama ilivyo kwa viongozi na watendaji wa TFF. Ni wazi Sendeu akiwa ofisa wa Yanga anajua taratibu za kufanya pale klabu yake isiporidhishwa na uamuzi wa mwamuzi au suala lingine lolote.
Matamshi ya Sendeu yanalenga kuchochea chuki na vurugu katika mpira wa miguu ambapo ni kinyume na Ibara ya 53(1) na (2) ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

KAMATI YA MISS TANZANIA YAWAOMBA RADHI WAZANZIBARI!

Hashim Lundenga - Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Tanzania.

Usiku wa kuamkia jumamosi ya tarehe 10 / 09 2011 tukio kubwa na la huzuni lilitokea huko Zanzibar ambapo wananchi wengi walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa wakati walipopatwa na ajali ya kuzama kwa MELI iliyokuwa ikitoka Unguja kuelekea Pemba .
Kwa bahati mbaya siku hiyo ya Jumamosi taaasisi yetu ilikuwa inahitimisha Fainali za Taifa za Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania 2011.
Kama waandaaji wa Mashindano haya na wenye Mamlaka kamili ya maamuzi juu ya ama kuendelea au la kuahirisha jambo hili, tulipatwa na mshituko mkubwa sana juu ya tukio hilo .
kamati yetu ilikaa na kutakafari katika tukio hilo kwa kuzingatia mambo yafuatayo:-
· Taarifa kamili ya maafa haya tuliipata rasmi saa tisa na nusu mchana ( 9:30 ) siku ya jumamosi ambayo ilikuwa ni masaa machache kabla ya Fainali za Miss Tanzania kuanza katika ukumbi wa Mlimani City .
· Wenzetu wa TFF waliendelea na mechi za ligi kuu ikiwemo ya Yanga na Ruvu Shooting.
· Katika kumbi za starehe ikiwemo mabaa na burudani za muziki wa bendi na kumbi za disco ziliendelea kama kawaida.
· Muda uliokuwa umebaki kuwakilisha jina la mshiriki wetu kwenye fainali za Miss World zilikuwa zimekwisha hivyo kulikuwa na hatari ya kupoteza nafasi hiyo
· Pia tamko rasmi la kusimamisha shughuli zote za burudani lilianza tarehe 11 septemba 2011 kuomboleza Kitaifa maafa hayo.
Hata hivyo kama waandaaji tulifanya shindano tukiwa katika maombolezo kwani kabla ya kuanza shindano Watu wote waliokuwepo ukumbini walisimama kimya kwa dakika moja na hata washiriki walipoingia kwenye jukwaa kwa mara ya kwanza walikuwa wamevaa vitambaa vyeusi katika mikono yao ikiashilia maombolezo.
Hali hii imetupa mkanganyiko na kujikuta tukiendelea na mashindano kitu ambacho tunaona tumewakosea Watanzania wenzetu.
Kama Waandaaji tunapenda kusistiza kwamba tunawajibika kwa hayo yaliyotokea na si Taasisi yeyote au Kampuni yeyote na tunaomba ichukuliwe kama ni makosa ya kibinaadamu hasa ukizingatia mazingira magumu tuliyokuwa nayo kwa wakati huo na mkanganyiko wa matukio na taarifa za tatizo hilo.
KUOMBA RADHI
Hata hivyo shughuli hiyo inawezekana imewakwaza watu wengi na kwa sababu hiyo na pia hali halisi ya janga hilo na kwa niaba ya viongozi wenzangu na wadau wa shughuli zetu tunatoa tamko la dhati kwa Familia za ndugu wote walikumbwa na maafa haya, wale wote walionusurika katika ajali hii na Watanzania wote kwa ujumla, kwamba TUNAWAOMBA RADHI KWA MKANGANYIKO ULIOTUTOKEA HADI KUFIKIA HALI HII. Hatuna neno zaidi ya kusema na kusisitizaTUNAOMBA RADHI
Mwenyezi MUNGU aziweke roho za marehemu mahali pema peponi,
Amina,
Hashim Lundenga
Mkurugenzi.

TWIGA STARS WATOLEWA ALL AFRICA GAMES

Timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars imetolewa katika michuano ya All African game kufuatia kutoka sare na Zimbabwe hapo jana.
Twiga stars imetolewa baada ya kujikusanyia pointi 2 kwa kutoka sare na Afrika Kusini huku wakichapwa na Ghana goli 2-1 katika mchezo wa ufunguzi.

VIINGILIO MECHI ZA CHAMAZI VYAWEKA HADHARANI

Timu za Simba na Yanga zitaanza kuutumia Uwanja wa Azam Chamazi ulioko Mbande, Dar es Salaam wiki hii. Septemba 14 mwaka huu Simba itakuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma wakati siku inayofuata African Lyon itakuwa mwenyeji wa Yanga.
 
Viingilio kwa mechi zinazohusisha timu za Yanga na Simba kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 7,000 tu vitakuwa sh. 15,000 kwa jukwaa kuu na sh. 5,000 mzunguko.
 
Kwa timu nyingine za Dar es Salaam zinazotumia uwanja huo kiingilio kitaendelea kuwa kile kile cha sh. 10,000 jukwaa kuu na sh. 3,000 mzunguko.

TANGAZO LA ZANTEL KWA WANAOTAKA KUCHANGIA, KUTOA NA KUPATA TAARIFA KUHUSU KUZAMA KWA MELI YA MV. SPICE ISLANDERS

Kwa kutoa taarifa za maiti zilizopatikana, kupata taarifa za abiria waliopotea katika ajali ya meli Spice Islanders piga kwa wahusika namba ya bure 0775112112.


 
Changia Mfuko wa Zanzibar kwa kutuma neno ZNZ kwenda 15580. Utatozwa kiasi cha Tsh 200 kwa kila SMS. Tuma SMS nyingi kwa kuchangia zaidi.

Monday, September 12, 2011

UMOJA WA WAISLAM WAISHIO UINGEREZA WASOMA DUA KUWAOMBEA WAATHIRIKA WA AJALI YA MELI YA MV. SPICE ISLANDERS

Baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Uingereza wakisoma dua ya pomoja kuwaombea waathirika wa meli ya MV. Spice Islandes iliyokuwa ikitokea Dar-es-Salaam kupitia Unguja kwenda Pemba usiku wa kuamkia tarehe 10 Septemba 2011. Idadi ya wtu waliopoteza maisha mpaka sasa ni 197 huku zaidi ya 600 wakiokolewa, juhudi za uokozi bado zinaendelea kwa ushirikiano wa Polisi wa Baharini kutoka nchini Afrika Kusini.


DK. SHEIN AONGOZA MAMIA KATIKA DUA YA KUWAOMBEA WAATHIRIKA WA MELI YA MV SPICE ISLANDES

 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete(watatu kutoka kushoto) akijumuika na baadhi ya viongozi wa Serikali na wananchi wa Zanzibar katika dua ya pamoja ya kuwaombea marehemu waliofariki katika ajali ya meli iliyotokea mwishoni mwa wiki eneo la Nungwi,Unguja.Viongozi wengine katika picha kutoka kushoto ni Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Seif Shariff Hamad,kushoto kwa Rais Kikwete ni Rais wa Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein,Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mohammed Gharib Bilal,Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Rais Mstaafu awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi.
Baadhi ya wananchi wa Zanzibar wakiswali wkati wa dua maalumu ya kuwaombea marehemu waliofariki katika ajali ya meli ya Spice Islander iliyotokea mwishoni mwa wiki eneo la Nungwi,Unguja.Swala hiyo ya pamoja ilifanyika leo(sept 12) katika viwanja vya Maisara.

WAZIRI NUNDU ATOA SALAMU ZA RAMBI RAMBI KWA RAIS WA ZANZIBAR

Waziri wa Uchukuzi  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Omar Rashidi Nundu.

Waziri wa Uchukuzi Mhe.Omar Rashidi Nundu,ametoa salamu za Rambi Rambi kutokana na vifo vya watu zaidi ya 200 vilivyotokea katika eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyotokana na kuzama kwa Meli ya Mv Spice .
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari kwa niaba ya Katibu Mkuu Edward Mkiaru, Waziri Nundu alisema, Wizara imepokea taarifa hiyo kwa masikitiko na inawapa pole wafiwa wote pamoja na kuwaombea afya njema wale wote walionusurika katika ajali hiyo.
Aidha wizara imewashukuru wananchi wote walioshiriki kwa njia moja ama nyingine katika kuokoa wale waliofikwa na mkasa huo.
“Kutokana na tukio hili tunamuomba Mwenyezi Mungu awafariji wote waliofikwa katika kipindi hiki kigumu na pia azilaze roho za Marehemu wa ajali hiyo mahali pema peponi”alisema Mkiaru

SIMBA, AZAM ZAINGIZA MIL 72

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Azam na Simba iliyochezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 72,167,000.
 
Watazamaji waliokata tiketi kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo walikuwa 21,129. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 15,000, sh. 7,000, sh. 5,000 na sh. 3,000.
 
Viti vya bluu na kijani ambavyo kiingilio kilikuwa sh. 3,000 viliingiza watazamaji 18,586, hivyo kuingiza sh. 55,758,000.

YANGA, RUVU SHOOTING ZAINGIZA MILIONI 23,388,000.

Kikosi cha Yanga
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 23,388,000.

Watazamaji waliokata tiketi kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo walikuwa 6,566. Viingilio vilikuwa sh. 15,000, sh. 7,000, sh. 5,000 na sh. 3,000.

MAMAAAAAAAAAAAA! TFF TENA.........

Ili kutekeleza maagizo ya Serikali kucheza mechi mbili tu za Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tumefanya marekebisho kwa baadhi ya mechi zilizokuwa zichezwe kwenye uwanja huo.
 Sasa mechi zitakazochezwa Uwanja wa Taifa ni – mechi namba 39- Azam vs Yanga (Septemba 18), mechi namba 50- Simba vs Mtibwa Sugar (Septemba 25), mechi namba 52- Yanga vs Coastal Union (Septemba 28) na mechi namba 58- Yanga vs Kagera Sugar (Oktoba 13).
 Nyingine ni mechi namba 62- Simba vs African Lyon (Oktoba 16), mechi namba 65- Yanga vs Toto Africans (Oktoba 20), mechi namba 72- Simba vs JKT Ruvu (Oktoba 22), mechi namba 78- Ynga vs Simba (Oktoba 29) na mechi namba 86- Moro United vs Simba (Novemba 2).
 Mechi zifuatazo zitachezwa Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam; mechi namba 35- Simba vs Polisi Dodoma (Septemba 14), mechi namba 29- African Lyon v Yanga (Septemba 15), mechi namba 45- Yanga vs Villa Squad (Septemba 21), mechi namba 66- Simba vs Ruvu Shooting (Oktoba 19) na mechi namba 71- Yanga vs Oljoro JKT (Oktoba 23).
.Uongozi wa Azam unaomiliki uwanja wa Chamazi tayari umekubali timu za Simba na Yanga kutumia uwanja huo kwa mechi hizo.

WAZAMIAJI KUTOKA AFRIKA KUSINI WATUA ZANZIBAR KWA AJILI YA UOKOZI!

Meli ya MV. SPICE ambayo imezama ikiwa na abiria wasioljulikana

Wazamiaji 12 kutoka nchini Afrika ya Kusini, wamewasili usiku huu mjini Zanzibar kuungana na wazamiaji wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini ili kufanya uhakiki wa kujua kama bado kuna mili iliyokwama kwenye Meli ya MV Spice Islander iliyozama chini ya bahari eneo la Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja usiku wa Jumamosi wiki iliyopita.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mh. Aboud Mohammed, amesema kuwa wazamiaji hao wamewasili wakiwa na zana za kisasa za uzamiaji na kwamba kazi ya kwanza itakayofanywa na timu hiyo ni kuhakikisha kuwa wanaifikia meli hiyo iliyozama umbali wa karibu nusu kimometa kwenye mkondo mkubwa wa maji na majabali.
Bado Serikali na wananchi mbalimbali wanadhani kuna miili ya watu waliokwama katika vyumba vya meli hiyo tangu ilipozama usiku wa Jumamosi Septemba 10 mwaka huu ikiwa na idadi ya watu isiyojulikana.
Makundi ya wananchi wamekuwa wakitaja idadi ya ndugu na jamaa waliosafiri na Meli hiyo na ambao hawajapatikana wakiwa hai ama miili yao kiasi cha kutia shaka kuwa huenda bado wamenasa ndani ya vyumba vya meli hiyo iliyozama chini ya kina kirefu cha mkondo wa bahari ya Hindi.
Tangu kuokolewa kwa abiria 619 na kuopolewa kwa miili ya watu 197 hadi jana jioni, hakujapatikana mtu hai ama mwili wa abiria aliyekufa maji ukielea juu ya maji ama kukokotwa kupelekwa mwambao mwa nchi kavu.
Katika eneo ilipo Meli hiyo zipo Meli nyingine za MV Kasa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na MV Mamba ya Jeshi la Polisi ambazo zote ziliwasili alfajiri siku ambayo tukio hilo la kuzama kwa MV Spice Islander.

TAARIFA KWA WATUMIAJI WA BLOG HII: TUTAKUWA TUKIWAPA HABARI MBALI MBALI AMBAZO ZINAHUSU AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA MV SPICE ISLANDERS

Katika kipindi hiki kigumu cha Msiba mzito BLOG yako ya COCOSPORT inatoa mkono wa Pole kwa Wazanzibari wote kwa jumla kwa msiba huu na kuwataka wawe na subira na kushirikiana katika kuendelea na uokowaji kwa kuweka ghadhabu na lawama upande na kupeana kila taarifa inayohusu tokeo hili kwa haraka.
Innaa lillaaahi wa innaaa ilayhi rajiuuun.
KWA NIABA YA WAFANYAKAZI WOTE WA COCONUT FM, (88.2) TUNASEMA TUKO PAMOJA KATIKA KPINDI HICHI KIGUMU MWENYEZI MUNGU AZILAZE ROHO ZA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI AAAMEN! PIA WAPE MOYO WA SUBRA WAFIWA WOTE NA MAJERUHI AWAJAALIE WAPONE KWA HARAKA.

Saturday, September 10, 2011

KUFUATIA AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA MV SPICE: DK. ALI MOHAMMED SHEIN ATANGAZA SIKU TATU ZA MAOMBOLEZO.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK Ali Mohammed Shein, ametangaza siku tatu za maombolezo kufuatia msiba mkubwa ulioikumba zanzibar kutokana na ajali ya meli iliyokuwa ikitokea Unguja ikielekea Pemba , iliyotokea usiku wa kuamkia leo.
Akitoa taarifa hiyo mbele ya vyombo vya habari leo jioni, huko Ikulu mjini Zanzibar DK Shein amesema Serikali inatangaza siku tatu za maombolezo kuanzia kesho tarehe 11 September, aidha katika kipindi hicho sherehe na tafrija zote hazina budi kusitishwa sambamba na bendera kupepea nusu mlingoti.
Akielezea mikakati ya Serikali katika msiba huo amesema serikali itashughulikia kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuwatambua waliofariki,kuwasaidia waliookolewa na waliopata maumivu, itashughulikia maziko kwa wale wote waliofariki kwa wale watakao tambuliwa.
Aidha DK Shein amesema kwa wale ambao hawatatambuliwa na jamaa zao Serikali itachukua jukumu la kuwazika katiaka lililotengea huko KAMA wilaya ya Magharibi Unguja.
Rais alivipongeza vikosi vya ulinzi kwa kazi nzuri waliofanya katika harakati za uokozi wakishirikiana na Wananchi, pamoja na vyombo vya habari ambavyo vimefanya kazi ya ziada ya kuwajuulisha wananchi matokeo yote ya ajali hiyo.
Aliwataka wananchi wote na zaidi waliofiwa kuwa wastahamilivu kwa msiba huo uliowafika na waone kuwa hayo ni majaala ya Mwenyezi Mungu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, mara baada ya kuzungumza na vyombo vya habari alitembelea eneo la Maisara ambapo maiti za wahanga hao wa ajali ya meli wanapofikia ili kutambuliwa na jamaa zao.
Wakati huo huo mpaka hivi sasa watu wapatao 620 wameokolewa wakiwa hai na watu 189 wamefariki dunia hata hivyo hali ya uokozi inaendelea.