Per Mertesacker
Mlinzi wa Werder Bremen anayechezea timu ya taifa ya Ujerumani Per Mertesacker anakaribia kufanyiwa uchunguzi wa afya yake katika klabu ya Arsenal.
Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 26- ambaye pia ni nahodha wa klabu hiyo ya Werder Bremen inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani maarufu Bundesliga, pamoja ya kwamba yumo katika kikosi cha timu ya taifa hivi sasa, ameruhusiwa kusafiri hadi London.Mipango ya Arsenal kumsajili Mertesacker, mwenye urefu wa futi 6 na inchi 6 aliyekwishacheza mechi 75 kwa timu ya taifa ya Ujerumani, inaweza ikawa ndio mwisho kwa klabu hiyo kutaka kumsajili mlinzi wa Bolton Gary Cahill.
Lakini Gunners pia wamo mbioni kumsajili beki wa kushoto Mbrazil Andre Santos.
Hatua ya wa meneja wa Arsenal Arsene Wenger kuimarisha safu yake ya ulinzi, imetokana na timu hiyo kuadhiriwa kwa kuchapwa mabao 8-2 na Manchester United siku ya Jumapili katika Ligi Kuu ya England.
Hivi karibuni klabu hiyo ilimuuza mlinzi wake wa kushoto Gael Clichy kwa Manchester City, na mlinzi wa kuume Emmanuel Eboue kwa klabu ya Uturuki ya Galatasary, wakati siku ya Jumanne imemuuza Armand Traore kwa klabu ya Queens Park Rangers.
Mlinzi wa kati wa Arsenal Thomas Vermaelen aliumia akijiandaa kwa safari ya Old Trafford na msimu uliopita hakuweza karibu msimu mzima akiwa ameumia kifundo cha mguu.
Mertesacker alikuwemo katika kikosi cha Ujerumani kilichoilaza England mabao 4-1 katika Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwaka 2010.
Na ameitwa tena katika kikosi cha Ujerumani kitakachopambana na Austria katika mechi ya kufuzu kwa Ubingwa wa Ulaya siku ya Ijumaa baada ya kuumia kisigino mwishoni mwa msimu uliopita.
No comments:
Post a Comment