Tuesday, August 23, 2011

BAADA YA UWANJA WA TAIFA KUFUNGWA SIMBA WAENDA TANGA, YANGA MJI KASORO BAHARI, TFF YASHINDWA KUFANYA MAREKEBISHO YA RATIBA YA LIGI KUU!


 Kikosi cha Yanga 2011/2012
Kikosi cha Simba 2011/2012


Baada ya Serikali kuufunga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya marekebisho, Yanga na Simba ambazo awali zilikuwa zimeruhusiwa kutumia uwanja huo kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zililazimika kutafuta viwanja vipya. Simba imehamia Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Yango iko Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
 
Licha ya timu hizo kupata viwanja vipya ratiba itabaki kama ilivyotolewa awali. Mechi za Simba zilizokuwa zichezwe Uwanja wa Taifa sasa zitachezwa Mkwakwani wakati za Yanga zitachezwa Jamhuri. Kutokana na mabadiliko hayo ratiba inasomeka kuwa Septemba 7 mwaka huu Coastal Union v Moro United (Mkwakwani) na pia Simba v Villa Squad (Mkwakwani). Mechi ya Simba v Villa Squad imesogezwa mbele kwa siku moja ambapo sasa itachezwa Septemba 8 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
 
MCHEZAJI CASTORY MUMBARA
TFF imeshindwa kumpa leseni Castory Mumbara ambaye ameombewa usajili katika timu ya Toto Africans kutokana na kutokuwa na Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) ambayo inatakiwa kutolewa kupitia mfumo wa mtandao wa Transfer Matching System (TMS).
 
Ikumbukwe kuwa Mumbara alikuwa akichezea timu ya Himalayan Sharpa ya Nepal ambapo alikwenda huko baada ya TFF kumpatia ITC. Hivyo ili aichezee Toto Africans, klabu hiyo ilipaswa kumuombea hati hiyo kupitia mtandao wa TMS baada ya kufanya mawasiliano na Himalayan Sharpa.
 
Muda wa usajili ulimalizika Julai 31 mwaka huu, hivyo Toto Africans kwa sasa haiwezi kumtumia mchezaji huyo badala yake inatakiwa kusubiri dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa tena Novemba mwaka huu. TFF iliendesha mafunzo ya kutumia mfumo wa TMS kwa watendaji wote wa klabu za Ligi Kuu ikiwemo Toto Africans.
 
MECHI YA STARS v ALGERIA
Mechi hiyo namba 103 ya mchujo kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani Equatorial Guinea na Gabon itachezwa nchini Septemba 3 mwaka huu.
 
Bado tunasubiri majibu ya ombi letu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo la kuturuhusu kutumia Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo.
 
ALL AFRICA GAMES
Mwamuzi msaidizi John Kanyenye wa Tanzania ni miongoni mwa waamuzi 32 (waamuzi wa kati na wasaidizi) walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha michezo ya All Africa Games itakayofanyika Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3-18 mwaka huu. Kati ya hao, 16 ni wanaume na 16 ni wanawake.
 
Kanyenye ni mmoja kati ya waamuzi watatu kutoka  ukanda wa CECAFA- Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati walioteuliwa kuchezesha michezo hiyo. Wengine ni mwamuzi wa kati wa kike kutoka Uganda, Nabikko Ssemambo na mwamuzi msaidizi wa kike kutoka Ethiopia, Trhas Gebreyohanis.

No comments:

Post a Comment