Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepeleka mashtaka mbele ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi dhidi ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu.
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Agosti 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine iliiagiza Sekretarieti kupeleka mashtaka hayo kutokana na kauli za viongozi hao kabla ya mechi ya Yanga na Simba iliyochezwa Agosti 17 mwaka huu.
Rage alikaririwa na vyombo vya habari kuwa Simba haitapeleka timu uwanjani kama mchezaji wake Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati hataruhusiwa kucheza, na kuwa ofisa mmoja wa TFF ndiye kikwazo kwa uhamisho wa mchezaji huyo.
Naye Sendeu kupitia vyombo vya habari alikaririwa kuwa Yanga haitaingiza timu uwanjani hadi itakapolipwa sh. milioni 16 inazoidai TFF ingawa deni hilo halikuwa na uhusiano na mechi hiyo ya Ngao ya Jamii.
Kauli hizo si tu zililenga kuvuruga mechi hiyo kwa kuwachanganya mashabiki, bali zilikuwa za kudhalilisha mchezo wa mpira wa mpira wa miguu.
Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi inayoongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) mstaafu Alfred Tibaigana itakuwa na kikao Agosti 28 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine itajadili mashtaka dhidi ya viongozi hao.
No comments:
Post a Comment