MZUNGUKO wa pili Ligi Kuu Tanzania bara umemalizika juzi kwa michezo 14 kuchezwa mikoa tofauti na kushuhudia mabao 23 yakifungwa na kadi 7 nyekundu zikitolewa na waamuzi wa ligi hiyo.
Klabu za Simba na Toto African zinaongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kushinda mechi zao mbili na kufikisha pointi sita kila moja lakini zikitofautiana kwa mabao ya kufunga. Wageni Patrick Mafisango wa Simba na Enyinna Darlinton wa Toto African ya Mwanza wanaongoza kwenye ligi hiyo baada ya kila mmoja kupachika mabao mawili.
Wakati huohuo jumla ya kadi 7 nyekundu zimetolewa tangu pazia la ligi hiyo lilipofunguliwa rasmi Jumamosi iliyopita na kushuhudia wachezaji Felix Sunzu (Simba), Salum Abubakar (Azam), Juma Seif 'Kijiko' (Yanga), Sunday Frank (Kagera), Mohamed Seleman (Villa), Omary Juma (Oljoro) na Shaban Ibrahim (Ruvu Shooting) wakilimwa kadi nyekundu. Idadi kubwa ya kadi zilizotolewa na waamuzi wa Ligi Kuu zinatokana na makosa ya utovu wa kinidhamu kwa wachezaji katika mchezo.
Katika hatua nyingine klabu nne mpya zilizopanda Ligi Kuu msimu huu zimeonyesha udhaifu kwa wakongwe wa ligi baada ya kukubali kugawa pointi 18 kwa wapinzani wao. Ni baada ya JKT Oljoro kujikusanyia pointi tatu badala ya sita, Coastal Union ya Tanga moja kama ilivyo kwa timu za Moro United na Villa Squad kwa michezo miwili zilizocheza mpaka sasa.
Wageni hao wa ligi wamekusanya pointi sita na kuacha 18 zikienda kwa wakongwe, endapo timu hizo zingeshinda michezo yote zingefikisha pointi 24 kwa kila mmoja kuwa na pointi sita.
No comments:
Post a Comment