Tuesday, September 13, 2011

LOUIS SENDEU ASHITAKIWA TENA!

Louis Sendeu - Afisa Habari wa Klabu ya Yanga.

Sekretarieti ya TFF itawasilisha mashtaka dhidi ya Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi inayoongozwa na Kamishna wa Polisi mstaafu Alfred Tibaigana kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi.
Mara baada ya mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Sendeu aliita mkutano na waandishi wa habari na kumshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao.
Aliongeza kuwa anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba, kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima si halali na alifanya hivyo kwa lengo la kuisadia Simba ili iendelee kukaa kileleni mwa ligi.
Kauli ya Sendeu ililenga kumjengea chuki Mahagi mbele ya mashabiki wa Yanga kama ilivyo kwa viongozi na watendaji wa TFF. Ni wazi Sendeu akiwa ofisa wa Yanga anajua taratibu za kufanya pale klabu yake isiporidhishwa na uamuzi wa mwamuzi au suala lingine lolote.
Matamshi ya Sendeu yanalenga kuchochea chuki na vurugu katika mpira wa miguu ambapo ni kinyume na Ibara ya 53(1) na (2) ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

No comments:

Post a Comment