Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK Ali Mohammed Shein, ametangaza siku tatu za maombolezo kufuatia msiba mkubwa ulioikumba zanzibar kutokana na ajali ya meli iliyokuwa ikitokea Unguja ikielekea Pemba , iliyotokea usiku wa kuamkia leo. Akitoa taarifa hiyo mbele ya vyombo vya habari leo jioni, huko Ikulu mjini Zanzibar DK Shein amesema Serikali inatangaza siku tatu za maombolezo kuanzia kesho tarehe 11 September, aidha katika kipindi hicho sherehe na tafrija zote hazina budi kusitishwa sambamba na bendera kupepea nusu mlingoti.
Akielezea mikakati ya Serikali katika msiba huo amesema serikali itashughulikia kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuwatambua waliofariki,kuwasaidia waliookolewa na waliopata maumivu, itashughulikia maziko kwa wale wote waliofariki kwa wale watakao tambuliwa.
Aidha DK Shein amesema kwa wale ambao hawatatambuliwa na jamaa zao Serikali itachukua jukumu la kuwazika katiaka lililotengea huko KAMA wilaya ya Magharibi Unguja.
Rais alivipongeza vikosi vya ulinzi kwa kazi nzuri waliofanya katika harakati za uokozi wakishirikiana na Wananchi, pamoja na vyombo vya habari ambavyo vimefanya kazi ya ziada ya kuwajuulisha wananchi matokeo yote ya ajali hiyo.
Aliwataka wananchi wote na zaidi waliofiwa kuwa wastahamilivu kwa msiba huo uliowafika na waone kuwa hayo ni majaala ya Mwenyezi Mungu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, mara baada ya kuzungumza na vyombo vya habari alitembelea eneo la Maisara ambapo maiti za wahanga hao wa ajali ya meli wanapofikia ili kutambuliwa na jamaa zao.
Wakati huo huo mpaka hivi sasa watu wapatao 620 wameokolewa wakiwa hai na watu 189 wamefariki dunia hata hivyo hali ya uokozi inaendelea.
No comments:
Post a Comment