Sunday, July 15, 2012

TAARIFA KUTOKA TFF, LEO, JULAI 15, 2012!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Julai 15, 2012
NGORONGORO, RWANDA KUUMANA JULAI 16

Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) itacheza mechi ya kirafiki na Rwanda itakayofanyika kesho (Julai 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya kujipima nguvu kwa Ngorongoro Heroes inayofundishwa na Kocha Jakob Michelsen kabla ya kucheza na Nigeria katika mechi za mchujo za michuano ya Afrika itaanza saa 10 kamili jioni.
Ngorongoro Heroes ambayo katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo iliitoa Sudan itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili Julai 29 mwaka huu dhidi ya Nigeria kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Rwanda ambayo inaundwa na wachezaji wengi waliocheza fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 miaka mitatu iliyopita tayari iko nchini. Kikosi chake kina wachezaji 20 na viongozi saba.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A itakuwa sh. 10,000.

MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
Mjumbe wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Dk. James Sekajugo atakuwa na mkutano na waandishi wa habari leo mchana (Julai 15 mwaka huu).
Mkutano huo utafanyika saa 8 mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Dk. Sekajugo kutoka Uganda yuko nchini kusimamia upimaji umri (MRI Test) kwa wachezaji wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) uliofanyika jana kwenye hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Upimaji huo umefanyika kutokana na maagizo ya CAF kuwa wachezaji wote wanaoshiriki michuano ya Afrika kwa umri chini ya miaka 17 ni lazima wapimwe kipimo cha MRI Test ndipo waruhusiwe kucheza.
Serengeti Boys imepangiwa kucheza Septemba mwaka huu dhidi ya Kenya katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment